Mke wa mwanajeshi auwawa kinyama kisha mwili kuswekwa kwenye ndoo ya maji, polisi wamsaka muuwaji



Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi mkali kuwatafuta waliohusika kufanikisha mauaji ya kinyama ya Samira Masoud (34), ambaye ni mke wa mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni (SACP) Susan Kaganda.
Samira aliuawa nyumbani kwake, eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam, na kisha mwili wa marehemu kukutwa ukiwa kwenye chombo kikubwa cha kuwekea maji cha namna ya beseni.
Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SACP Susan Kaganda, alisema mwili wa Samira ulikutwa Jumanne ya wiki hii baada ya taarifa kupatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu, ambaye ni mke wa mwanajeshi wa JWTZ (jina linahifadhiwa).
Akisimulia zaidi, Kamanda Kaganda alisema kuwa Jumanne ya wiki hii, majira ya saa 11:00 jioni, ndugu wa marehemu walifika katika kituo cha polisi kutoa taarifa kuhusu marehemu ambaye ni dada yao.
Alisema ndugu hao waliwaeleza polisi kuwa, kwa muda mrefu walikuwa hawana mawasiliano na dada yao, lakini siku hiyo (Jumanne), walipokea ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi ya Samira.
Kamanda alisema ujumbe huo ulikuwa ukisomeka kuwa, “Nendeni mkachukue maiti ya ndugu yenu… itaozea ndani.”
Alisema baada ya kuona ujumbe huo, ndugu hao walikwenda nyumbani kwa marehemu, lakini hawakuingia ndani baada ya kukuta gari lake lipo nje ya uzio. Waliamua kwenda kutoa taarifa polisi.
Aidha, alisema baada ya taarifa hiyo, polisi kwa kushirikiana na ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kibamba, walifika eneo hilo na kuvunja nyumba na ndipo walipokuta mwili wa marehemu kwenye chombo cha maji huku ukiwa umeharibika vibaya.
“Tumejaribu kila mara kuipiga simu ya marehemu ambayo ilitumika kutuma ujumbe kwa ndugu wa marehemu, lakini imezimwa…mume wake ambaye ni mwanajeshi wa JWTZ, ambaye alikuwa kwenye mafunzo ya kijeshi visiwani Zanzibar, alikuja baada ya kupewa taarifa za kifo cha mke wake. Hivi sasa bado hakuna anayeshikiliwa,” alisema Kamanda Kaganda.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwamba, hivi sasa wanasubiri ripoti ya daktari ili kujua kwa kina namna Samira alivyouawa.
Share on Google Plus

About Mr PinkMoja@ TZ

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 maoni:

Chapisha Maoni

ANDIKA MAONI YAKO HAPA