Rais
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari Polisi 8 waliouawa kwa
kushambuliwa na watu wenye silaha jana jioni katika eneo la Jaribu
Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Askari
Polisi hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria na wameshambuliwa kwa
kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es
Salaam – Lindi.
Mhe.
Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi
wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimeshtushwa
na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu 8 ambao wamepoteza
maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia za marehemu wote,
Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha
huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha,
Mhe. Dkt. Magufuli amelaani tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia
askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na
mali na ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha
vitendo hivyo.
Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA