WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka ya serikali za mitaa, wizara na
taasisi zote zitoe taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na
utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila robo mwaka.
Ametoa
agizo hilo leo jioni (Jumatano, Aprili 12, 2017) Bungeni mjini Dodoma
wakati akitoa maelezo ya kuhitimisha majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
Waziri
Mkuu alikuwa akijibu hoja ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe ambaye aliitaka Serikali itoe maagizo kwa
Wakurugenzi wote wa Halmashauri kutengeneza ajira angalau 20,000 kila
mwaka katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri zao, na
taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye
Bunge la Bajeti.
“Napenda,
kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi ya mwaka 2015, Ibara ya 59 inazielekeza Mamlaka za Serikali za
Mitaa zote nchini kuzingatia viashiria vya ukuzaji ajira katika mipango
ya maendeleo ya ngazi husika pamoja na kutoa taarifa za mwenendo wa
ajira kila robo mwaka,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema maelekezo hayo, yanazingatiwa katika Mwongozo wa kuandaa
Bajeti ya Serikali unaotolewa na HAZINA kila mwaka ambao unazitaka
Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote zibainishe fursa za
ajira zinazotarajiwa kupatikana kila mwaka kutokana na utekelezaji wa
miradi ya maendeleo.
“Vilevile
mwongozo huo unazitaka taasisi hizo kutoa taarifa za ajira
zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo kila robo mwaka.
Ninatoa agizo, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote
ziendelee kuzingatia maelekezo haya,” amesema.
Akizungumzia
kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema ndani ya mwaka mmoja,
jumla ya viwanda 2,169 vimesajiliwa vikiwemo viwanda vya mbolea, saruji,
chuma na vya usindikaji wa mazao.
“Serikali
pia inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuvutia uwekezaji
nchini. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda nchini ni dhahiri na tayari
tumeanza kuona matokeo. Kwa mfano, mkoa wa Pwani peke yake una viwanda
vikubwa 83 na vingine vidogo vidogo zaidi ya 200. Huu ndio mwelekeo wa
Serikali ya Awamu ya Tano,” amesisitiza.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama alisema
Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha
Vijijini (MIVARF) ilipanga kukarabati barabara zenye jumla ya kilomita
148.5, kujenga masoko manne na kukarabati kituo kimoja cha mafunzo ya
utunzaji mazao baada ya kuvuna.
Akijibu
hoja za utekelezaji wa programu hiyo kwa upande wa Pemba na Unguja,
Waziri Mhagama alisema miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ilianza
Agosti na Novemba 2014 na kazi hiyo kwa Pemba ilikamilika Desemba 2015
wakati kwa upande wa Unguja ilikamilika Januari 2016.
“Kazi
za ujenzi wa masoko ya Kinyasini na Mombasa (Unguja) pamoja na Konde na
Tibirinzi (Pemba) zilianza Desemba 2016 na zinatarajiwa kukamilika
Julai 2017. Wakandarasi wamehimizwa kuhakikisha wanakamilisha kazi hizo
katika muda uliopangwa ili kuendana na ratiba iliyopangwa,” alisema.
Akijibu
hoja kuhusu uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, Waziri Mhagama alisema
uamuzi wa kuhamia Dodoma na kuifanya Makao Makuu ya Serikali ilikuwa ni
ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alitaka
kuona Dodoma ikistawi na Serikali kuweza kuhamia huko ili kutekeleza kwa
vitendo dhana ya Mji Mkuu.
Alisema
uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma siyo suala la kisiasa kama baadhi ya
watu wanavyodai bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili kama
yalivyoelekezwa kwenye Ibara ya 151 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka
2015 na kama ilivyotamkwa kwenye GN namba 273 ambayo ni tamko la
Serikali na sheria halali.
Naye
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Anthony Mavunde alisema
kila mwaka vijana kati ya 800,000 hadi milioni moja wanaingia kwenye
soko la ajira wakati soko la ajira ni dogo.
Hata
hivyo, Naibu Waziri Mavunde alisema Serikali imeanza kubadilisha
mtazamo wa vijana kuhusu ajira kwani wengi wao hudhani kwamba kuwa na
ajira ni lazima mtu avae tai, awe na ofisi yenye meza na kiti
kinachozunguka.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA