Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake, kwa bajeti nzuri iliyowasilishwa jana tarehe 08 Juni, 2017 Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango.
Mhe.
Dkt. Lu Youqing ametoa pongezi hizo leo tarehe 09 Juni, 2017 Ikulu
Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Mhe. Rais
Magufuli ambapo amesema bajeti iliyowasilishwa imeakisi dhamira ya
kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa
miundombinu na ujenzi wa viwanda.
Ameongeza
kuwa pamoja na kuwasilishwa kwa bajeti nzuri, uchumi wa Tanzania
umeendelea kuwa imara na hivyo kuwavutia wadau wengi wa maendeleo
wakiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambao
wamekuwa wakishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa
ya maendeleo na yenye umuhimu mkubwa.
Mhe.
Dkt. Lu Youqing amebainisha kuwa Tanzania ni mahali pa kipaumbele kwa
uwekezaji kutoka China na kwamba Serikali ya China itaendelea
kuwashawishi wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza hapa nchini ili
kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kuzalishaji ajira nyingi zaidi kwa
Watanzania.
Amesema
katika bajeti ijayo, China itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa
kusaidia miradi inayohitajika kwa haraka katika maendeleo ya nchi, yenye
matokeo mazuri katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuongeza
ukusanyaji wa kodi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA