Na Veronica Simba – Biharamulo
Serikali
imetoa siku 14 kwa kampuni ya Stamigold, inayomiliki Mgodi wa Dhahabu
uliopo Biharamulo mkoani Kagera, kuandaa mpango mkakati wa kibiashara,
utakaobainisha namna itakavyojiendesha pasipo kuitegemea Serikali.
Agizo
hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon
Msanjila alipotembelea Mgodi huo na kuzungumza na Menejimenti pamoja na
wafanyakazi wake.
Profesa
Msanjila alisema kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Madini, ni
kuona Kampuni tanzu hiyo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
inajiendesha kibiashara na kiushindani ili ipate faida stahiki na
kulinufaisha Taifa kama ilivyo dhamira ya kuanzishwa kwake, na siyo
vinginevyo.
“Menejimenti
ya Kampuni, Bodi pamoja na Menejimenti ya STAMICO, nawapa hadi tarehe
21 mwezi huu, kila upande uwe umewasilisha mapendekezo ya kimkakati
yanayobainisha namna gani Stamigold itaweza kusimama yenyewe na
kujiendesha kiushindani kama zilivyo kampuni nyingine za kibiashara. Kwa
upande wetu, Kamishna wa Madini na mimi Katibu Mkuu pia tutakuja na
mapendekezo yetu.” alisema Profesa Msanjila.
Akifafanua
zaidi, Katibu Mkuu alisema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika
kampuni ya Stamigold hivyo haitakubali kuona mgodi huo unaendeshwa kwa
hasara. “Kila mtu awajibike kwenye eneo lake,” alisisitiza.
Alisema,
pamoja na kuwa Stamigold ni kampuni ya Serikali lakini imesajiliwa na
Taasisi inayotoa leseni za biashara ya Brela, hivyo inapaswa kujiendesha
kama kampuni nyingine za kibiashara.
“Kampuni
ya serikali ambayo haifanyi biashara haiendi kujiandikisha Brela. Ninyi
mnafanya biashara hivyo lazima mfanye kazi kibiashara.”
Aidha,
Profesa Msanjila aliutaka uongozi wa kampuni kuhakikisha unaweka wazi
taarifa zote za mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote ili waelewe
wanazalisha kiasi gani, wanapata faida kiasi gani, matumizi ni kiasi
gani na kama kuna hasara ibainishwe wazi.
Alifafanua
kuwa utaratibu wa kuweka wazi mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote
utaondoa manung’uniko kwani utaratibu wa kibiashara unamtaka mwajiri
amlipe mfanyakazi kulingana na mapato.
“Huwezi
kumlipa mtu mshahara hata pale ambapo hazalishi. Hii siyo sawa
kibiashara maana lazima utapata hasara. Huu ndiyo ukweli ndugu zangu.
Tubadilike. Hakuna hela ya kuchezea.”
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Mhandisi John Nayopa
alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa maagizo yote aliyoyatoa yatatekelezwa
ndani ya muda alioelekeza.
Aidha,
aliwataka wafanyakazi wa Stamigold kutoa ushirikiano kwa kutoa maoni na
ushauri wao wakati wa kuandaa mpango mkakati huo utakaoiwezesha Kampuni
kujiendesha kibiashara.
Katika
ziara hiyo, Katibu Mkuu aliambatana na viongozi wengine wa Wizara
akiwemo Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu, Miriam Mbaga, Kamishna
Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahaya
Samamba, Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kagera, Paschal Bundala na
Mhandisi Migodi kutoka wizarani, Kungulu Kasongi.
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA