Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii atembelea Makumbusho



Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda jumamosi tarehe 15 Juni, 2019 alitembelea Makumbusho ya Taifa kujionea urithi na hazina kubwa ya Taifa la Tanzania. Urithi huu wa utamaduni na asili ni pamoja na mafuvu na masalia ya binadamu wa kale au zamadamu, kama Australopithecus afarensis, Zinjanthropus (Paranthropus) boisei, Homo habilis, Homo erectus na Homo sapiens sapiens, yenye umri wa tangu miaka milioni 3.6 had miaka 200,000 iliyopita. 

Akiwa Makumbusho ya Taifa, Pof. Mkenda alijadiliana na kuielekeza Menejimenti ya Makumbusho ya Taifa hatua ambazo Wizara ya Maliasili na Utalii inachukua kuimarisha sekta ya malikale na hususan, Shirika la Makumbusho ya Taifa la Tanzania.

“Wizara inaiimarisha na kuijengea uwezo Makumbusho ya Taifa ili itimize majukumu yake ya msingi ya kutafiti, kuhifadhi, kuonesha na kuelimisha umma juu ya urithi wa Taifa na dunia kwa ujumla”.

Prof. Mkenda, aliyasema hayo alipotembelea chumba maalumu cha kuhifadhia mikusanyo adhimu, na kujionea masalia hayo ya binadamu wa kale, hati ya Uhuru wa Tanganyika, tai ya uhuru, kinyago maarufu cha kimakonde na chungu, mchanga na vibuyu halisi vilivyotumiwa na Baba wa Taifa Mwal. Julius K. Nyerere kuchanganya mchanga kama ishara ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964.

Prof. Mkenda alisema kuwa kufika kwake Makumbusho ya Taifa inadhihirisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imejipambanua na inajali na kuthamini urithi wa Taifa na iko tayari kuulinda urithi huu kwa gharama yoyote kwa sababu ukipotea haupatikani tena.

“Vitu hivi ni muhimu na ni urithi wetu, hivyo tunatakiwa kuvitunza kwa gharama yoyote kwani ni utambulisho wa Taifa la Tanzania, vinaleta amani, mshikamano, uzalendo na furaha. Aidha, vinavutia watalii wa ndani na nje na hivyo kuongeza pato la Taifa”, alisema Prof. Mkenda.

Akizungumza na menejemeti na baadhi ya wataalamu wa Makumbusho ya Taifa Prof. Mkenda ameweka wazi kuridhishwa na uhifadhi na kazi iliyofanywa na Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na Ofisi ya Usalama wa Majengo ya Serikali ya kukiimarisha chumba hicho maalumu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa na Menejimenti yake kuimarisha zaidi uhifadhi na ulinzi wa urithi huu wa nchi yetu na dunia kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Fuvu la Zinjanthropus lenye umri wa miaka milioni 1.75 iliyopita liligunduliwa kwenye bonde la Olduvai, Ngorongoro tarehe 17 July, 1959 na wataalamu wa Akiolojia Dkt. Louis Leakey na mke wake Dkt. Mary Leakey.

Uguduzi huo ulibadilisha uelewa wa wanasayansi kuhusu mchango wa bara la Afrika katika sayansi ya chimbuko la binadamu duniani. Masalia ya Zinjanthropus (Paranthropus) boisei pamoja na masalia mengine ya binadamu wa kale (kama Homo habilis, Homo erectus), zana zao za mawe na masalia ya mifupa ya wanyama waliyokula bonde la Olduvai miaka milioni 2.0-1.0 iliyopita, vinathibitishia dunia kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee yenye taarifa bora na sahihi kuhusu chimbuko la binadamu na utamaduni wake (tabia, teknolojia, chakula na namna ya kupata chakula hicho) katika kipindi hicho; na kwamba bonde la Olduvai ndilo Chimbuko la Binadamu wote duniani (the Cradle of Humankind).

Prof. Mkenda ameitaka Makumbusho ya Taifa kuanzisha kampeni ya kutangaza vivutio mbalimbali ambavyo vinapatikana katika makumbusho zetu yakiwemo masalia ya binadamu wa kale.

“Elimu hii na vitu nilivyoviona leo nimefurahi sana, lakini Watanzania wangapi wanavijua? Serikali ya Awamu ya tano inajipambanua kujali na kujivunia vitu vyetu, lugha yetu ya Kiswahili, maliasili zetu, malikale zetu na utamaduni wetu, alisema Prof Mkenda..

Alisema matangazo kwenye luninga, redio na magazeti kuhusu vitu vinavyotunzwa Makumbusho ya Taifa, yatajenga uelewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa makumbusho na hivyo, kufanya watu wengi kuja kutembelea makumbusho zetu.

“Msipotangaza hakuna anayewezea kujua kuwa vitu muhimu kama hivi viko hapa Makumbusho ya Taifa, tunatakiwa tuwaambie wananchi ili waje kuviona,” alisisitiza.

Prof. Mkenda alisema, “tunapoelekea kwenye maadhimisho ya miaka 60 tangu kugunduliwa kwa fuvu la Zinjanthropus, fuvu hilo, halitaondolewa Makumbusho ya Taifa kwenda bonde la Olduvai, bali litaendelea kuhifadhiwa na kutunzwa vizuri Makumbusho ya Taifa na badala yake nakala itatumika pale inapohitajika.

Aidha, amesisitiza kuwa matangazo hayo yawe ya ndani na nje ya nchi (International Promotion) kwa sababu kuna watafiti wengi nje ya Tanzania ambao wangependa kuja kufanya utafiti katika Nyanja za akiolojia na paleontolojia.

Sambamba na hilo, aliwaagiza Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Freddy Manongi na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Prof. Audax Mabulla, kuisimamia Kamati inayohusika na maandalizi ya maadhimisho hayo kubuni na kupanga matukio mbali mbali yatakayoleta hamasa katika kuadhimisha miaka 60 ya ugunduzi wa Zinjanthropus na kutangaza vivutio mbalimbali vilivyoko Tanzania.

Alisisitiza kuwa matukio tofauti yaandaliwe kuanzia mwezi Julai mpaka Desemba mwaka huu kama sehemu ya kumbukumbu ya ugunduzi wa fuvu la Zinjanthropus boisei.
 
Share on Google Plus

About Mr PinkMoja@ TZ

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 maoni:

Chapisha Maoni

ANDIKA MAONI YAKO HAPA