Picha: Jinsi wachimbaji 15 walivyokikwepa kifo baada ya kufukiwa kwa siku 4 kwenye kifusi mgodini Geita;mr.pinkmoja.com
Wakiwa wameloa mwili mzima na tope la udongo mwekundu wa mgodini uliokuwa umezifunika nguo zao, wachimbaji hawa 15, hawakuamini macho yao baada ya kuliona tena jua kwa mara ya kwanza, kufuatia kuwa chini ya ardhi, kwa siku nne mfululizo.
Miili yao haikuwa na nguvu, tumboni hakukuwa na kitu na njaa ya siku nne ilikuwa imewatafuna vilivyo kiasi cha kushindwa kusimama kwa miguu yao miwili baada ya kuokolewa.
Kutenganishwa na mazingira ya kawaida ya dunia na kuwa chini ya kifusi cha mgodi ambako harufu ya kifo ilianza kuwa dhahiri kwenye pua zao, ni mkasa utakaobaki daima vichwani mwao na utakuwa kama mkanda wa video utakaojirudia kucheza vichwani mwao kwa miaka mingi.
Na sasa wakiendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya mkoani Geita, baada ya kupewa huduma ya kwanza punde walipookolewa, wanaendelea kukusanya nguvu, na pale zitakapowaijia, bila shaka watahitaji muda wa kutafakari mustakabali wao baada ya kukikwepa kifo, katika shimo lenye udongo uso na huruma.
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA