Baada
ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kubomoa baadhi ya nyumba
zilizowekewa kinga ya muda, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imesema hilo
ni kosa la kuupuza amri ya mahakamana na kueleza hatua ambazo
waathirika wanapaswa kuzichukua.
Msajili
wa mahakama hiyo, Frank Mahimbali jana alisema kuwa wanachoweza kufanya
waathirika ni kwenda mahakamani kuomba iwaite waliohusika na ubomoaji
huo ili wajieleze ni kwa nini wasifungwe kwa kupuuza amri ya mahakama.
Mahimbali alisema mtuhumiwa akitiwa hatiani anaweza kufungwa jela.
Ijumaa
iliyopita, mahakama hiyo ilitoa amri ya zuio la muda la ubomoaji kwa
nyumba 286 zilizoko katika operesheni ya bomoabomoa maeneo mbalimbali
kati ya Ubungo Maji na Kiluvya, zilizojengwa ndani ya umbali wa mita
121.5 kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro.
Amri
hiyo ilitolewa na Jaji Leila Mgonya baada ya maombi ya dharura
yaliyowasilishwa na wakazi 286 wa maeneo hayo, wakiomba mahakama itoe
zuio nyumba zao zisibomolewa kusubiri kesi yao ya msingi itakapoamuriwa.
Hata
hivyo, juzi Tanroads ilibomoa nyumba tatu katika eneo la Kimara Stop
Over, ambazo ni kati ya hizo 286. Nyumba hizo zilizobomolewa ni pamoja
na Nicomed Leo na ya Aisha Juma.
Wakati
mahakama ikitoa msimamo na maelekezo hayo kwa waathirika wa bomoabomoa
hiyo ambao nyumba zao zimewekewa kinga hiyo, wakili wao Benedicto
Mandele alisema jana kuwa tayari wameshamwandikia barua Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), kueleza malalamiko yao na hatua wanazopanga
kuzichukua.
Wakili
Mandele alisema katika barua hiyo ambayo pia nakala yake imetumwa kwa
Jaji Mgonya, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Saalam, Ofisa Mtendaji wa
Tanroads, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi
Kinondoni, wateja wake wameeleza kusikitishwa kwao na kitendo hicho
wakati kuna amri ambayo ilibandikwa kwenye nyumba hizo.
“Tayari
barua hiyo imepokewa leo (jana) saa nne na sasa hapa ninaandaa maombi
kwa ajili ya kumuita meneja wa mkoa wa Tanroads afike mahakamani
kujieleza ni kwa nini asifungwe jela kama mfungwa wa kesi ya madai kwa
kupuuza amri ya mahakama,” alisema Wakili Mandele na kuongeza kuwa
maombi hayo dhidi ya meneja huyo wa Tanroads atapeleka mahakamani leo
baada ya wateja wake kuweka saini.
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA