Gavana
mteule wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema
amepokea kwa heshima kubwa dhamana aliyopewa na Rais John Magufuli na
anatambua changamoto za nafasi hiyo.
Profesa
Luoga ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) - Taaluma, amesema leo Jumatatu Oktoba 23,2017 kuwa atatumia
wataalamu wa BoT kufanya kazi.
Amesema anahitaji ushirikiano wa kila mtu katika kufanikisha kazi aliyopewa.
“Nimepokea
kwa heshima dhamana niliyopewa nikitambua kwamba zipo changamoto.
Nitakwenda kujifunza zaidi kwa sababu sijawahi kuwa Gavana, nitatumia
wataalamu waliopo katika kutekeleza majukumu yangu,” amesema Profesa
Luoga.
Rais
Magufuli Julai 11,2017 alimteua Profesa Luoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi
ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akichukua nafasi ya Bernard Mchomvu
ambaye uteuzi wake ulitenguliwa Novemba mwaka jana na bodi hiyo
kuvunjwa.
Profesa
Luoga ni mtaalamu katika masuala ya sheria za kodi na amefundisha
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu mwaka 1986 kabla ya
kupandishwa cheo na kuwa profesa mshiriki (Associate Professor) mwaka
2005.
Ameshika
nafasi mbalimbali chuoni hapo ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa kamati
ya misaada ya kisheria katika kitivo cha sheria mwaka 1993 - 1995,
mkurugenzi wa masomo ya shahada za awali (2005 - 2009), katibu wa baraza
la chuo kikuu (2009 - 2013) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma
(2013 hadi sasa).
Profesa
Luoga aliyezaliwa mwaka 1958 ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Alihitimu shahada ya kwanza ya sheria UDSM mwaka 1985. Baadaye alikwenda
kusoma Shahada ya Uzamili (LLM) katika chuo cha Queen’s University cha
Canada (1988).
Mwaka
1988 alihitimu Shahada ya Uzamili ya Sheria za Kimataifa (MIL) katika
Chuo cha Lund University cha Sweden (1991) na Shahada ya Uzamivu (PhD)
katika Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza mwaka 2003.
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA