Licha
ya kupata hasara kwenye robo ya tatu ya mwaka, kampuni ya Barrick
imetenga dola 300 milioni za Marekani (zaidi ya Sh660 bilioni) kuilipa
Serikali, lakini imeweka sharti; inataka iruhusiwe kusafirisha
makinikia.
Acacia,
kampuni tanzu ya Barrick na inayomiliki migodi ya Bulyanhulu na
Buzwagi, imezuiwa tangu mwezi Machi kusafirisha mchanga huo wa madini
kwenda kuuyeyusha nje ya nchi kwa ajili ya kupata mabaki ya dhahabu,
shaba, fedha na madini mengine yaliyoshindikana kuchenjuliwa migodini.
Baada
ya majadiliano baina ya Serikali na Barrick, kampuni hiyo ya Canada
ilikubali kulipa dola 300 milioni “kuonyesha uaminifu”.
Taarifa
ya miezi mitatu ya Barrick (Julai-Septemba) iliyotolewa juzi,
inaonyesha kuwa ilipata hasara ya dola 11 milioni (zaidi ya Sh24
bilioni) tofauti na faida ya dola 175 milioni (zaidi ya Sh385 bilioni)
iliyopata katika kipindi kama hicho mwaka jana (dola moja ya Kimarekani
ni sawa na takriban Sh2,200 za Tanzania).
“Kupungua
kwa mapato kunatokana na kushuka kwa uzalishaji na bei ya dhahabu
pamoja na zuio la kusafirisha makinikia ambalo Serikali ya Tanzania
iliiwekea Acacia,” inasema ripoti hiyo.
Vilevile,
Barrick inasema kupungua kwa mapato yake kumechangiwa na ongezeko la
makadirio ya kodi yanayofika dola 172 milioni (zaidi ya Sh378 bilioni)
zilizopendekezwa kwenye majadiliano ya mustakabali wa operesheni za
Acacia nchini.
Wakati
Barrick ikitenga kiasi hicho cha kodi, Acacia ina dola 128 milioni
(zaidi ya Sh282 bilioni) na kufanya jumla ya dola 300 milioni
zilizokubaliwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika kwa miezi mitatu
iliyopita.
Masharti
hayo si ya kwanza, itakumbukwa kwamba siku chache baada ya mkutano wa
kukabidhi ripoti ya majadiliano hayo, kampuni ya Acacia ilisema haiwezi
kulipa Dola 300 milioni kwa mkupuo na kwamba Barrick inajua hilo.
Ofisa
fedha mkuu wa Acacia, Andrew Wray alinukuliwa na vyombo vya habari
akisema: “Hatuna huo uwezo kuilipa Tanzania ili tumalizane kwenye
mgogoro wa kodi uliopo.”
Wray
alisema hayo Oktoba 20 wakati Acacia ilipokuwa ikiwasilisha ripoti yake
ya fedha kwa robo ya tatu ya mwaka iliyoishia Septemba, ikionyesha
kushuka kwa mapato na faida ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka
jana.
Barrick
imeiunga mkono Acacia kwenye msimamo wake kuhusu malipo hayo ya dola
300 milioni ikisema: “Kutokana na hali ya Acacia kifedha, malipo haya
yanapaswa kufanywa kwa awamu yakitegemea mauzo ya dhahabu na
usafirishaji wa makinikia.”
Katika
robo hiyo ya tatu, faida ya Acacia imeshuka kwa asilimia 70 kutoka dola
52.878 milioni (zaidi ya Sh116.331 bilioni) mpaka dola 16.038 (zaidi ya
Sh35.283 bilioni).
Wakati
wa mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Ikulu, Waziri wa Katiba na
Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alikuwa mwenyekiti wa
wawakilishi wa Serikali alisema Barrick wamekubali kutekeleza masharti
yote ya sheria mpya ya madini.
Lakini
kwenye taarifa yake, kampuni hiyo inasema itaendelea kuzungumza na
Serikali ili kuondoa zuio la kusafirisha makinikia na kwamba mazungumzo
hayo yataenda sambamba na kutafuta suluhu ya deni la kodi la kiasi cha
dola 190 bilioni (zaidi ya Sh424 trilioni) ambazo Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imeitoza Acacia ikiwa ni malimbikizo ya kodi, faini na
riba.
“Tunatarajia mazungumzo haya yatakamilika ndani ya nusu ya kwanza ya mwaka ujao,” inasema Barrick.
Pamoja
na hasara hiyo ya robo ya tatu, kwa miezi yote tisa, Barrick imepata
faida ya dola 1.752 bilioni (zaidi ya Sh3.854 trilioni) ambayo ni zaidi
ya mara saba ikilinganishwa na iliyopata kwa muda kama huo mwaka jana.
Mwaka uliopita, ilitangaza faida ya dola 230 milioni (zaidi ya Sh506
bilioni).
Mbali
na taarifa hiyo ya fedha, Barrick imefafanua kwa wadau wake kuhusu
makubaliano yaliyoafikiwa kwenye majadiliano ya miezi mitatu baina yake
na Serikali.
Chanzo: Mwananchi
0 maoni:
Chapisha Maoni
ANDIKA MAONI YAKO HAPA